KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 29 June 2012


Madaktari Bingwa Nao Wagoma



TUKIO la kutekwa nyara, kupigwa na kujeruhiwa vibaya, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, limechochea kasi ya mgomo baada ya madaktari bingwa kutangaza kujitosa rasmi kwenye mgogoro huo.Awali madaktari hao hawakushiriki mgomo huo, lakini jana walieleza kwa nyakati tofauti kuwa, wameamua kuungana na wenzao kutokana na unyama aliofanyiwa kiongozi wao akiwa katika harakati za kutetea na kupigania haki zao.

Madaktari hao wa hospitali za Muhimbili, Moi, KCMC, Mbeya, Bugando na Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuwa wameingia kwenye mgomo huo kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali kutoa tamko kuhusu utata wa tukio hilo.

Tukio hilo la aina yake kutokea nchini, limeathiri upatikanaji wa huduma zote za matibabu katika hospitali hizo, huku madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Moi, wakielekeza nguvu zao kunusuru maisha ya mwenzao aliyeumizwa.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mgomo huo utaendelea hadi hapo Serikali itakapotekeleza madai yao.

"Tunaitaka Serikali kuacha vitisho kwa madaktari nchini, tunaitaka itambue kwamba mgogoro huu hauwezi kumalizwa kwa njia yoyote vikiwemo vitisho bali ni kwa kukaa meza ya majadiliano na kukubaliana na madaktari," alisema Dk Chitega na kuongeza:

"Ninawashukuru madaktari wote nchi nzima, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya kwa ujumla wao kwa kusitisha huduma baada ya kupigwa mwenzetu. Tunaomba mshikamano huu uendelee," alisema Dk Chitega.

Gazeti hili lilishuhudia wagonjwa wakiwa wamekaa katika makundi bila kujua la kufanya, huku wengine wakiamua kuondoka na kwenda hospitali binafsi.

Waliliambia Mwananchi kwamba kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kuungana na madaktari hao kuitaka Serikali kutatua mgogoro huo haraka.

Wagonjwa waliofika katika eneo hili pia walielezwa bayana na maofisa wa Moi kwamba huduma zimesitishwa kutokana na madaktari kugoma.

Ocean Road

Madaktari bingwa katika Taasisi ya Ocean Road nao waligoma kutoa huduma hatua iliyozua taharuki kwa wagonjwa waliofika kwa ajili ya matibabu.

Gazeti hili lilishuhudia ofisi za madaktari hao zikiwa zimefungwa na hata zile ambazo zilikuwa wazi, madaktari hawakuwapo.

Mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Dachi, alisema kuwa, wagonjwa wengi wamekuwa wakiandikishwa mapokezi, lakini wanachukua muda mrefu kumuona daktari.


Mgomo huo pia umeendelea katika Hospitali ya Amana wilayani Ilala huku uongozi wa hospitali hiyo ambao uligoma kuzungumza na vyombo vya habari, ukihaha kunusuru hali hiyo.

Katika Hospitali za Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.

Mbeya

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ,madaktari bingwa ambao awali hawakugoma jana waliingia kwenye mgomo na kusababisha wagonjwa katika hospitali hiyo hususan kitengo cha wazazi, kusota bila matibabu.

Habari kutoka katika hospitali hiyo zilieleza kuwa hivi sasa madaktari bingwa wanatoa huduma kwa kujuana.

Mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kitendo alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya yao kimewakatisha tamaa.

Alisema kuwa, hali hiyo sasa imehamia hadi katika Kituo cha Wazazi cha Meta na kufafanua kuwa hali ni mbaya, tayari wajawazito wametakiwa kuhamia katika Hospitali ya Mkoa ambayo imefurika wagonjwa.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa, Dk Eliuter Samky hakuweza kuzungumzia tukio hilo jana kutokana na kile kilichoelezwa na katibu wake muhtasi kwamba ana kazi nyingi.

Mwanza
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mkoani Mwanza nao wamegoma, huku kiongozi wa Kamati Ndogo ya hospitali hiyo inayoshughulikia migomo, akikataa kuzungumzia hali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu baada ya kutoonekana katika maeneo ya hospitali, mmoja wa viongozi wa Kamati hiyo, Dk Geogre Adrian, alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi suala hilo na kwamba kufanya hivyo, ni kwenda kinyume na maagizo aliyopewa na Kamati Kuu.


Akizungumzia huduma katika hospitali hiyo alisema kuwa hajui lolote kwa kuwa hawajagusa maeneo ya kazi kwani wapo kwenye mgomo.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia huduma katika hospitali yake, hakupatikana.

Watimuliwa
Jana Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Charles Majinge alitoa tangazo la kuwataka madaktari waliopo mafunzoni ‘Interns’ katika hospitali hiyo kurejea kazini na kama watakiuka agizo hilo, watakuwa wamejifukuzisha wenyewe.


Manyara
Mkoani Manyara, madaktari kumi katika Hospitali ya Haydom Wilaya ya Mbulu wamegoma tangu juzi.Idadi ya wagonjwa katika hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), inaongezeka siku hadi siku.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotaka kutajwa majina yao, madaktari hao ambao wanafanya mafunzo ya vitendo katika hospitali hiyo, wamesema kuwa hawatatibu wagonjwa mpaka madai yao yatekelezwe.


Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Anatory Choya, alithibitisha kutokea kwa mgomo huo na kufafanua kwamba wanaendelea kufanya mazungumzo ili kupata ufumbuzi.

Choya alisema kuwa madaktari wanaoendelea na kazi, wameelemewa kutokana na wagonjwa kuwa wengi.

Alisema kati ya madaktari 11 wanaosoma kwa vitendo hospitalini hapo, mmoja tu anayesomeshwa na hospitali hiyo, ndiye hajagoma.

KCMC
Hali katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro imezidi kuwa tete na kuwafanya ndugu kuwahamishia wagonjwa wao katika hospitali binafsi.

Mwananchi lilitembelea wodi za hospitali hiyo na kukuta vitanda vikiwa wazi.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya madaktari ambao wapo kwenye mgomo kwa sharti la kutotajwa majina, walisema hawako tayari kurudi kazini kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Dodoma
Wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma jana walijikuta wakipata taabu baada ya madaktari wa hospitali hiyo kusitisha huduma kwa takriban saa sita kuanzia asubuhi.

Muda wa mchana utoaji huduma katika hospitali hiyo uliendelea ingawa kwa kusuasua.

Tofauti na siku zote, jana chumba cha daktari kilichokuwa wazi ni kimoja tu hali iliyosababisha msongamano mkubwa.

Arusha

Mjini Arusha, madaktari wameendelea na mgomo katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na kusababisha kudorora huduma huku wagonjwa kadhaa wakiondolewa hospitalini hapo.

Mgomo huo, ulianza saa 1 asubuhi hadi saa 6:00 mchana, ambapo madaktari na wauguzi,waligoma kutoa huduma wakitaka kujua hatima ya Dk Ulimboka. Walitaka pia kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo na waandishi wa habari, kuhusu mgogoro wao.

Askari anyimwa huduma
Askari wa Usalama Barabarani ambaye jina lake halikufahamika mara moja ambaye alipata ajali jana, alijikuta akishindwa kuhudumiwa katika hospitali ya Mount Meru na kuondolewa kutokana na mgomo huo.

Askari huyo, aliyevaa sare, alifikishwa hospitalini hapo saa 5:00 asubuhi akiwa kwenye teksi, lakini wauguzi waliokuwa zamu walishauri apelekwe sehemu nyingine.

Hata hivyo, uongozi wa hospitali ya mkoa, ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Omar Chande, jana ulifanya kazi ya ziada ya kuwabembeleza madaktari hao, kurejea kazini, kusubiri uamuzi wa Serikali.

Mgomo, Dk Ulimboka vyateka Bunge

Mgomo wa madaktari na kutekwa kisha kupigwa Dk Ulimboka jana vilitawala mjadala wa Bunge hadi pale Spika Anne Makinda alipotoa mwongozo kwamba suala hilo lisijadiliwe kwani liko mahakamani.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa juzi pale alipokuwa akizungumzia mgomo wa madaktari na kuhitimisha kwamba Serikali ilikuwa inajiandaa kutoa kauli na msimamo wake hivyo “liwalo na liwe’.

Pinda alilazimika kutoa maelezo kutokana na swali aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kufahamu maana ya kauli ya Waziri Mkuu ambayo aliita kuwa ni nzito na iliyozua mjadala mkali nchini.

Kadhalika, Mbowe alitaka kufahamu hatua ambazo Serikali imechukua kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma za tiba kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba madaktari katika hospitali kadhaa walikuwa wakiendelea na mgomo.

Kadhalika Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alimuuliza Pinda kwamba haoni kwamba ni busara kujiuzulu wadhifa wake kutokana na ahadi yake kwamba mgomo wa madaktari usingetokea, lakini ahadi hiyo imeshindwa kutekelezeka.

Akimjibu Mbowe, Pinda alikiri kutoa kauli hiyo ndani ya Bunge juzi na kusema alifanya hivyo akiamini kuwa jambo hilo lilikuwa mahakamani na akasema asingeweza kusema jambo lolote kwa kuwa hana tabia ya kuwa na utovu wa nidhamu wa kuingilia mambo ya mahakamani.

Hata hivyo, alijitetea kuwa kabla ya kutoa kauli hiyo bungeni juzi, hakuwa na taarifa kuhusu tukio la kupigwa kwa Ulimboka na akasema kuwa, kauli yake haihusiani kabisa na Serikali kuhusika katika jambo hilo kwa namna yoyote ile.

Waziri Mkuu alisema tayari amekwishaagiza vyombo husika kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya haraka ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki mara moja.

“Kwanza namtakia afya njema ndugu Ulimboka, na mimi nataka Watanzania waamini kuwa tulikuwa katika mazungumzo mazuri na madaktari chini yake Ulimboka hivyo tukio hilo ambalo limetokea katika mazingira magumu limetushtua kweli, kama ni Serikali basi ingekuwa ni Serikali ya ajabu kweli,’’alisema Pinda.

Kuhusu namna ya kusaidia Watanzania wasiathirike na mgomo huo, alisema tayari Serikali imeshaagiza madaktari kutoka wizarani kutumika na kuwaomba waliostaafu kutoa huduma katika kipindi hicho kigumu.

Mkakati mwingine ni pamoja na kutumia hospitali za Jeshi ikiwamo Lugalo waanze kutoa huduma hizo wakati Serikali inaendelea kuzungumza kwa utaratibu na madaktari.

Lissu aliuliza swali la nyongeza kumtaka Pinda kuachia ngazi hali iliyosababisha mvutano kwani Waziri Mkuu alikosoa uulizaji wa swali hilo kuwa halikustahili.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala la madaktari akitaka taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo ilifanyia kazi suala la mgomo wa madaktari ijadiliwe bungeni.

Hata hivyo, Spika Makinda alisema ripoti hiyo haiwezi kujadiliwa kwani tayari Serikali ilishakabidhiwa kwa ajili ya kuifanyia kazi na kwamba mapendekezo ya Bunge kupitia ripoti hiyo yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa.

Habari hii imeandaliwa na Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma, Godfrey Kahango,Mbeya, Joseph Lyimo,Mbulu, Sheilla Sezzy,Mwanza, Rehema Matowo, Moshi, Masoud Masasi,Dodoma, Fidelis Butahe, Geofrey Nyang'oro Dar, Mussa Juma, Arusha, Bakari Kiango na Victoria Mhagama.

No comments:

Post a Comment