KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday, 20 January 2011

WAZIRI CHAMI ATEMBELEA WAJASILIAMALI JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Cyril Chami ( Katikati) akiongea katika majumuisho ya ziara yake ya kuwatembelea wajasiriamali wa sekta ya viwanda vidogo wanaofanya shughuli katika maeneo mbali mbali Jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa SIDO na kulia kwake ni Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Viwanda Vidogo na vya kati katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Consolata Ishebabi.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Cyril Chami, amewataka wajasiriamali kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia ubora na mahitaji ya soko la bidhaa husika ili kufanya shughuli zao kuwa na tija.

Katika ziara yake ya siku moja jijini Dar es salaam, Waziri Chami amesema serikali inathamini mchango wa wajasiriamali katika uchumi wa nchi na kuwaahidi ushirikiano wa serikali katika kuwawezesha kwa kuwatafutia fursa za mafunzo, mitaji, masoko, malighafi na maeneo ya kufanyia kazi zao.

Aidha, amewaahidi wajasiriamali hao kuwa, Wizara yake kupitia SIDO itaandaa mafunzo hapa nchini na baadae ziara ya mafunzo nchini India ili kuwawezesha kujifunza kwa vitendo maendeleo makubwa ya kiteknolojia yaliyofikiwa nchini India.

Ziara hiyo ya Mh Waziri Dar es salaam ilianzia katika Mtaa wa Gerezani Kariakoo na kuendelea katika mtaa wa Tabata Dampo na kumalizikia katika eneo la Sido Vingunguti ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wajasiriamali wanatengeneza bidhaa mbali mbali katika maeneo hayo na kubadilishana nao mawazo.

Dkt Chami amewataka wajasiriamali hao hasa wanaozalisha bidhaa za chuma kutotumia kisingizio cha ukosefu wa malighafi ya chuma kama sababu ya kuharibu miundo mbinu ili kupata bidhaa hiyo.

Amesema serikali iko mbioni kuanza uvunaji wa chuma ghafi katika migodi ya madini hayo iliyopo eneo la Liganga Mkoani Iringa ili kuondoa kabisa tatizo la ukosefu wa chuma ghafi hapa nchini na kukomesha biashara haramu ya chuma chakavu inayovutia watu wasio waaminifu kufanya hujma ya kuharibu miundombinu.

Kwa upande wao wafanyabishara hao wameiomba serikali kutatua haraka tatizo la mgao wa Umeme na gharama kubwa za nishati hiyo zinazofanya shughulu zao kutokuwa na tija na kuiomba mamlaka ya mapato Tanzania TRA kuangalia uwezekano wa kuwaondolea kodi kubwa wanazotozwa wajasiriamali hao.

Katika ziara hiyo, Dkt Chami aliongozona na Mkurugenzi Mkuu wa EPZA Dkt Adelhelm Meru, Mwakilishi wa Kamishna wa TRA Bw Allan Kiula na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sido Bw Pius Wenga.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Cyril Chami akitazama mtambo wa kutengenezea bidhaa za nati na bolts zinazotengenezwa na wajasiriamali wadogo eneo la Vingunguti Sido.
Waziri wa Viwanda na biashara, Dkt. Cyril Chami akiongea na wajasiriamali katika eneo la Tabata dampo mara baada ya kuwatembelea hapo

No comments:

Post a Comment