Na Mary Kweka - MAELEZO
KAMPUNI ya Reli Nchini (TRL) imerejesha huduma ya usafiri wa reli ya kati kutoka mikoa ya Dar es salaam kwenda Kigoma na kuanzia leo ijumaa tarehe Januari 21, mwaka 2011.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo (jana) Mkuu wa Usafirishaji wa Reli hiyo Bw. Charles Ndenge usafiri huo umerejea baada ya kukamilika kwa ukarabati wa daraja lililopo kati ya stesheni za Bahi na Kintinku mkoani Dodoma.
“Huduma hii itaanza kwa kuzipitisha treni za mizigo zilizokuwa zimekwama katika mkoa wa Tabora kuja Dar es salaam na kwa sasa zitapita kwenye daraja hilo lililokarabatiwa na baadaye zitafuatiwa na treni ya abiria iliyotoka mkoa wa Kigoma jana joini kuja Dar-Es- Salaam ambayo imeshawasili Tabora” alisema Ndenge.
Aidha alisema kufuatia hatua hiyo, huduma ya usafiri wa treni ya abiria kutoka Dar es salaam kwenda kigoma inatarajia kuanza leo saa kumi na moja jioni ambapo treni nyingine kutoka Kigoma itafika Dar es salaam kesho Januari 22, 2011 majira ya saa mbili asubuhi.
Akifafanua zaidi alisema huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Dar es salaam kwenda kigoma itakuwa inatolewa mara mbili kwa wiki kwa siku za jumanne na ijumaa na inatajiwa kuanza rasmi januari 25, 2011.
Akizungumzia kuhusu huduma ya usafiri wa reli kanda ya ziwa mikoa ya ikiwemo mkoa Mwanza, alisema huduma hiyo bado haijaanza kutokana na kutokamilika kwa ukarabati wa mabehewa ya kutosha kusafirishia abiria na mizigo.
“Kwa usafiri wa Mwanza bado hatujajua tutaanza lini kwani tunaendelea kukarabati mabehewa ya abiria na mizigo ambapo yatakapokuwa tayari tutawatangazia wananchi na wadau wote wa usafiri wa reli ratiba nzima itakavyokuwa”
Kampuni ya Reli Tanzania ilisitisha kwa muda huduma zote za usafiri wa reli ya kati kuanzia januari 11 mwaka 2011 baada ya kuharibika kwa daraja lililoko kati ya stesheni za Bahi na Kintinku mkoani Dodoma ambapo mkondo wa maji uliharibu nguzo moja kati ya nne zilizokuwa zimeshikilia daraja hilo na kusababisha sehemu ya kati ya daraja kutitia.
No comments:
Post a Comment