KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Saturday, 22 January 2011

MAZIWA YA MGANDO NI DAWA YA KUPUNGUZA UNENE

 
Jumamosi, 22 January 2011

UTAFITI mpya umegundua kuwa, bakteria wanaopatikana katika maziwa ya mgando, mtindi na uji uliochacha vinaweza kufanya kazi mara mbili zaidi ya inayofanywa na vituo vya mazoezi (gym).

Matokeo ya utafiti huo yamekuja wakati mamilioni ya Watanzania wakihangaika kutafuta dawa na kufanya mazoezi ya aina mbalimbali ili kupunguza unene na uzito wa miili yao.

Utafiti huo uliotolewa hivi karibuni unaonyesha kuwa, bakteria rafiki, aitwaye ‘lactobacillus’ anayepatikana katika maziwa ya mtindi na vitu vingine vilivyochacha anao uwezo wa kupunguza unene na uzito kupita kiasi (obesity) na huzalisha kinga ya kuyeyusha mafuta ya ziada mwilini.

Dk David Mwaniki, Mwanasayansi kutoka Taasisi ya Utafiti ya nchini Kenya, alisema kuwa tangu mwaka uliopita wa 2010, wanasayansi wamejitahidi kuonyesha jinsi bakteria hao wanavyoweza kufanya kazi ya kumeng’enya mafuta katika mwili wa binadamu.

“Ninaamini kuwa, hii ni sehemu ya utafiti ambayo italeta mapinduzi katika kudhibiti fetma (obesity), vilevile jinsi virutubisho vyake vinavyofanya kazi nyingine za ziada,” alisema Mwaniki, ambaye taasisi yake imeonyesha hamasa ya kufanya utafiti kuhusu aina hiyo ya bakteria.

Wanasayansi hao walisema kuwa, watu wanaotoka katika jamii ambazo maziwa ya mtindi au uji ni sehemu ya mlo wao huwa wembamba kwa miili yao kutokana na aina hiyo ya bakteria.

"Wale wanaotumia maziwa ya mgando mara kwa mara au kwa muda mrefu wako katika nafasi ya kuwa na miili isiyo na mafuta pamoja na  kupunguza kasi ya kushambuliwa na magonjwa yanayosababishwa na viumbe mbalimbali," alisema Mwaniki.

Kaimu Mkurugenzi  wa Taasisi ya  Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR), Dk Charles Massaga  alisema, hana taarifa rasmi  kuhusu utafiti huo, lakini akasema anakusudia kufuatilia kwa karibu  ili ikiwezekana  jopo la watafiti wa hapa nchini nao wachunguze kwa undani kama kweli maziwa ya mtindi yana uwezo huo.

“Kwa sasa sina taarifa kama kweli, maziwa ya mtindi yana uwezo wa kupunguza mafuta mwilini kama mnavyodai, lakini kwa kuwa habari kama hizo ni za msingi kwa watafiti kama sisi, hatuna budi kuzifanyia kazi kuanzia sasa,’ alisema Dk Massaga.

Dk Massaga alisema kama bakteria hao wanaopatikana katika maziwa ya mtindi wana uwezo wa kufanya kazi kama zilivyotajwa na wanasayansi hao itakuwa ni moja kati ya tiba nyepesi na zisizo na gharama kubwa.

“Kama kweli bakteria wanaoishi katika maziwa ya mtindi wana uwezo wa  kupunguza uzito, kuzuia maambukizi mbalimbali, wakati huo huo bado ikawa  ni sehemu ya lishe tena ipatikanayo kwa urahisi basi itakuwa ni moja ya tiba za gharama nafuu na za muhimu,” alisema.

Dk Massaga aliongeza kwa kusema, kama nchi za Afrika zimeweza kuwa na wanasayansi wenye uwezo mkubwa kiasi hicho basi Afrika inatarajiwa kuwa tishio katika wakati huu ambapo sayansi na teknolojia ndiyo msingi wa kila kitu.

Hata hivyo, utafiti mwingine kama huo uliofanywa hivi karibuni na Profesa Jeremy Nicholson kutoka Chuo Kikuu cha Imperial nchini Uingereza unaonyesha kwamba, bakteria aina ya lactobacillus wana uwezo wa kupunguza kiasi cha mafuta kilichonyonywa na mwili, hivyo kuondoa uwezekano wa kupata fetma au unene kupindukia.

Kwa mujibu wa profesa huyo, bakteria hao muhimu huweza  pia kuweka makazi katika uke na utumbo, kisha kuteketeza wadudu waharibifu wanaojulikana kisayansi kama ‘probiotics’.

Probiotics ni viumbe hai wanaosaidia kuimarisha mmneng’enyo wa chakula, kudhibiti vijidudu vya maradhi katika utumbo mpana, kuzuia ukuaji wa bakteria wenye madhara na kuongeza nguvu ya kinga ya mwili.

Utafiti huo unaeleza kuwa bakteria hao, wana uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili na kumpa mwanadamu maisha yenye afya.

Dk Mwaniki alisema utafiti wa Profesa Nicholson na wenzake umeongeza vipengele muhimu katika vimelea hivyo vya probiotics ambavyo ni kuimarisha afya kwa watoto na watu wengine, hasa katika ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Alisema bakteria hao (lactobacillus) wana uwezo mara mbili wa kuzuia kuharisha na kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa watoto.

“Tumegundua kuwa, lactobacillus wana uwezo wa kubadilisha mimea midogomidogo katika utumbo na kuwafanya bakteria wanaosababisha madhara kwa watoto hata watu wazima wasiishi” alisema Dk Mwaniki.

Aliongeza kuwa: “cha kufanya kwa sasa, ni mataifa kuweka mipango ya  kuwaongeza bakteria hao na kuanzisha sheria za nchi ambazo zitaonyesha jinsi watakavyotumika kama sehemu ya mlo ili kuimarisha afya za watu.”

Mbali na tafiti hizo utafiti mwingine uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Taifa ya Afya nchini Marekani,(ANIH) umeonyesha kuwa bakteria wa probiotics wana uwezo wa kuzuia maambukizi ya VVU kwa watoto wakati wa kunyonyesha.

Wakati huo huo watafiti hao walisema, wanawake wenye kiasi kidogo cha asidi katika mazingira ya uke wana nafasi kubwa ya kupata maambukizi ya VVU kwa urahisi ukilinganisha na wale ambao sehemu zao hazina tatizo hilo.

Takwimu za utafiti huo zinaonyesha kuwa, asilimia 78 ya wanawake wasio na tindikali ya kutosha katika uke wanaweza kuambukizwa maradhi kwa haraka na kwamba tiba ya tatizo hilo ni kuongeza  bakteria wa lactobacillus.

Habari zinasema, wanasayansi  wanaendelea kushawishika kuwa matumizi ya bakteria wasio na madhara huenda ikawa ni njia nyepesi ya kuzuia maambukizi, kwa kuwaongeza bakteria hao katika vyakula kama maziwa, mtindi, sukari au hata unga tangu viwandani wakati wa uzalishaji.

No comments:

Post a Comment