KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Sunday, 4 March 2012

Mrithi Wa Dk.Migiro UN Huyu Hapa


Na Mwandishi Maalum

New York

Mwana-Diplomasia mkongwe na mzoefu katika tasnia ya Uhusiano wa Kimataifa, Bw. Jan Eliasson raia wa Sweden ndiye atakayeshika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ametangaza uteuzi wa Bw. Eliasson mbele ya waandishi wa habari mwishoni wa wiki, ambapo amesema Msweden huyo anayechukua nafasi itakayoachwa na Naibu Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Asha- Rose Migiro ataanza majukumu yake Julai Mosi mwaka huu.

Ban Ki Moon, amewaeleza waandishi kwamba, kama alivyowahi kusema huko nyuma, Naibu Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Asha- Rose Migiro ataendelea na wadhifa wake hadi mwezi june mwaka huu.

Kabla ya uteuzi wake, Bw. Jan Eliasson ambaye si mgeni katika Umoja wa Mataifa , amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Darfur, amewahi pia kuwa Rais wa Baraza kuu la 60 la Umoja wa mataifa, na amewahi pia kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu Haki za Binadamu.

Kwa sasa Bw. Eliasson anasimamia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs)

Aidha Bw. Jan Eliasson utumishi wa serikali yake amewahi pia kuwa Balozi aliyeiwakilisha nchi yake ( Sweden ) nchini Marekani, na New York, na amewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden.

Pamoja na kumtangaza Bw. Eliasson kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya, Ban Ki Moon pia amemtangaza Bi. Susana Malcorra raia wa Argentina kuwa Msimamizi Mkuu mpya wa Ofisi yake.

Kabla ya uteuzi huu Bi Malcorra alikuwa akiongoza Idara inayohusika na usambazaji wa vifaa na misaada katika Misheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa. Anachukua nafasi inayoachwa wazi na Bw, Vijay Nambiar ambaye anakuwa Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Myanmar.

Aidha katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Ban Ki Moon amebainisha kwamba uteuzi wa maafisa wengine wa ngazi za juu na ambao mchakato wake umekwisha kuanza watatangazwa baada ya taratibu za kuwapata kukamilika

No comments:

Post a Comment