SLAA, MKAPA KUONGOZA MAPAMBANO ARUMERU, NASSARI, SUMARI WAPITISHWA
Na Waandishi wetu, Dar na Arusha
VYAMA vya CCM na Chadema vimetangaza rasmi vita ya kuwania Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha huku vikianika majina ya makada watakaoongoza mapambano kwa ajili ya kujihakikishia ushindi.
CCM ambayo imempitisha Siyoi Sumari kuwania nafasi hiyo, imesema kampeni zake zitazinduliwa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho ambaye pia alikuwa Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa na Chadema itawatumia viongozi wake wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Wakati huohuo, Kamati Kuu (CC) ya Chadema jana ilimpitisha, Joshua Nasari kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe aliwaeleza viongozi wakuu wa chama hicho, wapenzi na wafuasi wa Chadema waliojazana eneo la Hoteli The Ice Age Usa-River, wilayani Arumeru jana kuwa wamejiandaa kikamilifu kunyakua jimbo hilo na kamwe hawatakubali hujuma zozote kutoka kwa mtu au chama chochote.
Mbowe aliyezungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wake, Dk Slaa kumtanga rasmi Nasari, alitamba kuwa mchakato wa kumtafuta mgombea kupitia chama hicho haujaacha nyufa wala mifarakano miongoni mwa wagombea na wafuasi wao kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya siasa ambavyo hakuvitaja.
Alisema mara nyingi mipasuko ndani ya vyama vya siasa hutokana na mchakato wa kupata wagombea kutokana na hila za baadhi ya viongozi, wanachama au wapambe wa wagombea, hali aliyosema haijajitokeza ndani ya Chadema kutokana na mfumo mzuri unaozingatia demokrasia kwa wote bila kujali umaarufu au ukwasi wa mtu.
“Wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu kuomba uteuzi tumewaalika katika Kamati Kuu na wote wameridhika na ushindi na uteuzi wa mgombea mwenzao na wote watashiriki kikamilifu kwenye kampeni kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana,” alisema Mbowe.
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu, Dk Slaa, alisema kikao hicho kilichoshirikisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya zinazoongozwa na Chadema, kwa kauli moja kilipitisha jina la Nasari kuitikia sauti ya wananchi na wakazi wa Arumeru waliomchagua kwa kura 805 kati ya 888 zilizopigwa kwenye kura za maoni.
“Wananchi Arumeru tumesikia kauli yenu kupitia kura zenu za maoni, Nasari ni kijana wenu siyo wa Dk Slaa, Mbowe wala Chadema.
Katika kura za maoni, Nasari alimwacha mbali mgombea wenzake Anna Mghiwa aliyemfuatia kwa kupata kura 23 huku wagombea wengine wanne, wakipata kura chini ya 20.
Chama hicho pia kinaendelea kufanya tathimini ya kutumia helikopta katika kampeni zake katika jimbo hilo.
Nasari ashukuru
Akitoa shukrani mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chake, Nasari aliwaomba wafuasi, wapenzi na wanachama wote wa Chadema kushikamana na kuwa tayari kwa mapambano ya haki, kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
"Wao (CCM), najua watatumia dola na fedha, lakini sisi tusihofu kwani tuna Mungu anayetupigania kwa sababu mapambano yetu ni kudai haki dhidi ya uovu.
Kwa pamoja tukishirikiana kuondoa hofu kwani tutashinda," alisema Nasari.
CCM
Kwa upande CCM Kamati Kuu (CC) ya chama hicho jana ilimteua Mwenyekiti mstaafu ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya Tatu , Mkapa, kuongoza kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa chama hicho, Siyoi Sumari katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alisema kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana, kilipitisha jina la Siyoi kuwania nafasi hiyo iliyoachwa na baba yake, Jeremia Sumari aliyefariki usiku wa Januari 18 mwaka huu.
Nape alieleza kwamba, kamati hiyo pia imemteua Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha ya chama hicho, Mwingilu Nchemba kuratibu kampeni hizo.
Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga ambao CCM ilishinda, Mkapa ndiye aliyefungua kampeni hizo huku, Nchemba akiratibu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Akizungumzia tuhuma za rushwa ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika mchakato wa uteuzi, aliitaka Takukuru kuhakikisha wanakamata mtandao mzima uliohusika na utoaji rushwa.
Kauli ya Siyoi
Sumari, aliambia Mwananchi Jumapili kuwa kwamba pamoja na kufurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake kupeperusha bendera ya CCM wilayani Arumeru Mashariki, chama hicho kinapaswa kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kinatetea jimbo hilo.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba changamoto zote alizozipitia katika mchakato wa uteuzi , zikiwemo tuhuma mbalimbali za rushwa ni misukosuko ya kisiasa ambayo haiwezi kuepukwa zaidi ya kukabiliana nayo.
“Nashukuru chama kwa kupitisha jina langu, lakini changaomoto zote nilizokuwa nikipitia naamini ni misukosuko tu ya kisiasa, lakini tusahau yaliyopita sasa tusonge mbele kunyakua ushindi,” alisema Sumari
UVCCM
Katika hatua nyingine Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM ) wilayani Arumeru, imefurahishwa na uamuzi uliofanywa na CC ya CCM kumpitisha Siyoi kupeperusha bendera ya chama hicho na kueleza kwamba kilio cha wanachama wa CCM wilayani humo, sasa kimesikilizwa.
Hata hivyo, wakati jumuiya hiyo ikiupokea ushindi huo kwa furaha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) imeendelea na kamata kamata yake ambapo safari hii ilimshikilia na kumhoji kwa muda Katibu Hamasa wa umoja huo wilayani Arumeru Mashariki, John Nyiti kisha kumwachia huru.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Esther Maleko alisema mbali na kilio cha wakazi wa jimbo hilo kusikika juu ya mgombea wao, umoja wao umejipanga kikamilifu kuingia ulingoni kuhakikisha ushindi unapatikana.
Hekaheka za uchaguzi wa jimbo hilo wakati zikiendelea baadhi ya makada wa CCM na UVCCM wilayani humo wameendelea kukumbwa na misukosuko baada ya viongozi wake akiwemo Nyiti kushikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wilayani humo.
Nyiti alipoulizwa juu ya taarifa hizo kwa njia ya simu alikiri kukamatwa na maofisa wa Taasisi hiyo.
Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto alipoulizwa na gazeti hili juu ya taarifa hizo hakuweza kukiri wala kukataa juu ya kuhojiwa kwa kada huyo na kudai kwamba wanaohojiwa na Taasisi hiyo wako wengi na wengine wanahojiwa kama mashahidi, hivyo alidai si vyema kuwataja majina kwa kuwa bado wanakamilisha uchunguzi wao.
Hali ilivyo ndani ya vyama
Makundi ya vigogo wa CCCM ambao wanajipanga kugombea Urais mwaka 2015, yametajwa kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho katika uteuzi wa mgombea wa Ubunge Arumeru Mashariki.
Mpasuko wa makundi hayo, inaelezwa unaweza kuchangia chama hicho kupoteza jimbo hilo.
Sumari amekuwa akiungwa mkono na kundi la Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa huku wagombea wengine, walikuwa wakiungwa mkono na kundi la na vigogo wa chama hicho wanaojipambanua kuwa ni wapiganaji dhidi ya ufisadi...Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment